Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fedha zitumwazo na wahamiaji kwa nchi zao ni mara tatu zaidi ya ODA- IFAD

Fedha zinazotumwa na wahamiaji waishio ugaibuni kwa  jamii nyumbani zinasaidia watu milion 800 ulimwenguni kote
Picha-IFAD
Fedha zinazotumwa na wahamiaji waishio ugaibuni kwa jamii nyumbani zinasaidia watu milion 800 ulimwenguni kote

Fedha zitumwazo na wahamiaji kwa nchi zao ni mara tatu zaidi ya ODA- IFAD

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Leo ni siku ya kimataifa ya utumaji fedha duniani, ambapo Umoja wa Mataifa unasema hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa ili fedha zinazotumwa na wahamiaji kwenye nchi zao za asili ziweze kuchangia maendeleo endelevu.

 

Umoja wa Mataifa unasema mwaka  2017, wahamiaji milioni 200 walituma jumla ya dola bilioni 481zilitumwa kwa nchi tegemezi zaidi kwa fedha hizo.
Dola bilioni 466 kati ya fedha hizo zilitumwa nchi zinazoendelea na kusaidia watu takribani milioni 800 kote ulimwenguni.
Kiasi hicho, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, ni mara tatu zaidi ya kiwango kinachotolewa na nchi kama misaada rasmi ya maendeleo, ODA.
Kutokana na mwelekeo huo, Gilbert F. Houngbo ambaye ni rais wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) amesema katika ujumbe wake kuwa kuna umuhimu wa kuendeleza  jitihada za kusaidia familia zinazopokea fedha hizo ili ziweze kujenga mustakabali wao endelevu na wa jamii zao.
Amesema kukiwepo na fursa sahihi za uwekezaji kulingana na mazingira na malengo yao, familia hizo zinazopokea fedha zinaweza kuwa mawakala wa mabadiliko katika jamii zao.
Mkuu huyo wa IFAD amesema ni kwa mantiki hiyo mwezi uliopita watunga sera zaidi ya 400 walikutana Malaysia na kupitisha mapendekezo kadhaa ya kuhakikisha fedha zinazotumwa kutoka ughaibuni zinakuwa kichochea kamili cha maendeleo.
Mapendekezo hayo ni pamoja na kuendeleza huduma za msingi za kifedha kama vile kuweka na kukopa ambazo kwazo familia zinaweza kutumia ili kuwa na matumizi bora ya fedha wanazopokea.
Halikadhalika kupunguzwa zaidi kwa gharama za utumaji fedha kwa kuwa takwimu zinaonyesha kuwa ingawa gharama hizo zimepunguzwa bado ni za juu, mfano ukitolewa kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara ambako gharama ni asilimia 9.3 ya fedha zilizotumwa.
Bwana Houngbo amesema hatua hizo ni muhimu kwa kuwa leo hii kiwango kikubwa cha fedha zinazotumwa hupokewa na kutumiwa papo hapo.
IFAD inakadiria kuwa dola bilioni 6.5 zitatumwa nchi zinazoendelea kati ya mwaka 2015 na 2030, zikihusisha watumaji na wapokeaji zaidi ya bilioni 1.
 
Karibu nusu ya fedha hizo zitaelekezwa maeneo ya vijijini ambako umaskini na njaa vimekithiri.
 
Mtu mmoja kati ya watu saba duniani hufaidika moja kwa moja na usaidizi huo wa kawaida wa kati ya dola 200 na 300 mara kadhaa kwa mwaka.

IFAD inasema wakati kiasi hiki  cha fedha kinaonekana kuwa kidogo kwa nchi zilizoendelea , mara nyingi ni sawa na  asilimia 50 au zaidi ya mapato ya familia ya wahamiaji katika nchi zao za asili.