Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mvua Somalia kutumbukiza watoto kwenye unyafuzi-UNICEF

Faylow, mwenye umri wa miaka minne, ni mmoja wa watoto 160,000 waliotibiwa kwa unyafuzi na UNICEF nchini Somalia
Picha ya UNICEF Somalia-Makundi
Faylow, mwenye umri wa miaka minne, ni mmoja wa watoto 160,000 waliotibiwa kwa unyafuzi na UNICEF nchini Somalia

Mvua Somalia kutumbukiza watoto kwenye unyafuzi-UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Mafuriko yanatokana na mvua zinazonyesha nchini Somalia, siyo tu yanasababisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao bali yanatishia mustakbali wa kiafya wa watoto.

Msemaji wa shirika linalowahudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, Christopher Boulierac amesema hayo leo mbele ya waandishi habari mjini Geneva Uswisi.

Bwana Boulierac amesema nusu ya watu wapatao 230,000 waliopoteza makazi yao tangu kuanza kwa mafuriko mwezi Aprili mwaka huu ni watoto.

Mvua haziwezi kukomesha mgogoro wa utapia mlo kwa watoto nchini Somalia.

Ameonya kuwa nusu ya watoto hao wenye umri wa chini ya miaka mitano, ambao idadi yao ni takriban  milioni 1.25 wanaweza kupata utapiamlo uliokithiri, ujulikanao pia kama unyafuzi.

Msemaji huyo wa UNICEF amesema kuwa mwaka huu pekee shirika lake limewatibu watoto zaidi ya 88,000 ambao walikuwa wakikabiliwa na unyafuzi.

Anasema mvua husambaza magonjwa ambayo ni hatari kwa watoto wenye utapiamlo kwani mfumo wao wa kinga ya kimwili huwa   imedhoofika.

Wakimbizi wa ndani wakimbilia Mogadishu Somalia wakitafuta msaada wa chakula na maji kufuatia ukame uliokithiri vijijini nchini humo.
Picha: OCHA
Wakimbizi wa ndani wakimbilia Mogadishu Somalia wakitafuta msaada wa chakula na maji kufuatia ukame uliokithiri vijijini nchini humo.

Ametaja magonjwa kama vile kuhara na kipindipindu ndio yanahofiwa kutokea.

UNICEF inaomba ufadhili zaidi iweze kuendelea kuhudumia watoto ambapo Bwana Boulierac amesema mwaka huu wamepokea dola milioni 24.3 tu kati ya dola milioni154.9 ilizoomba.

Pengo hilo ni sawa na asilimia 71.