Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi wa Ukraine wameteseka vya kutosha, suluhu ya kudumu lahitajika.

Rosemary DiCarlo, mkuu wa Idara ya masuala ya siasa ya Umoja wa Mataifa
Picha-UNTV
Rosemary DiCarlo, mkuu wa Idara ya masuala ya siasa ya Umoja wa Mataifa

Wananchi wa Ukraine wameteseka vya kutosha, suluhu ya kudumu lahitajika.

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekutana hii leo mjini New York, Marekani likiongozwa na waziri wa mambo ya nje wa Poland Czaputowicz, ambaye nchi yake ndio inashikilia urais wa baraza hilo kwa mwezi huu wa Mei.

Lengo la kikao lilikuwa kujadili mgogoro wa kivita uliodumu kwa zaidi ya miaka 5 nchini Ukraine.

Akihudubia Baraza la Usalama kwa mara ya kwanza tangu kupitishwa kwa azimio namba 2202 kuhusu utekelezaji wa mchakato wa amani kwa jina “makubaliano ya Minsk” mwezi Februari mwaka 2018, Bi Rosemary Dicarlo ambaye ni mkuu wa Idara ya masuala ya siasa ya Umoja wa Mataifa amesema ahadi za mara kwa mara kuhusu usitishwaji wa mapigano hazijazaa matunda ingawa mapigano yamepugua ikilinganiswa na mwaka 2015.

Ameongeza kuwa takwimu za hivi karibuni kutoka ofisi ya haki za bindamu ya Umoja wa Mataifa imebaini kuwa machafuko yanayoendelea nchini Ukraine yamesababisha zaidi ya raia 2,700 kupoteza maisha huku watu 9,000 wakijeruhiwa kutokana na makombora na mabomu ya ardhini hivyo kusababisha idadi ya wakimbizi wa ndani kufikia milioni 1.6 .

 

Kikao cha Baraza la Usalama
UN /Mark Garten
Kikao cha Baraza la Usalama

Aidha amesema, Umoja wa Mataifa unaendelea kuwa na wasiwasi kutokana na ripoti ya mwezi mei iliyowasilishwa na Bwana Ertugrul Apakan ambaye ni mkuu shirika la usalama na ushirikiano barani ulaya, ambayo imebaini kuwa hali ya kibinadamu nchini Ukraine hususani katika maeneo ya Donetsk ni hatarishi hivyo usitishwaji wa mapigano haraka iwezekanavyo ni muhimu ili kuokoa maisha ya maelfu ya raia wasio na hatia na pia miundombinu katika pande zote kinzani.

Mkuu huyo pia katika hotuba yake ameongeza kuwa kufuatia machafuko yanaoendela huko Ukraine misaada ya kibindamu inahitajika kwa zaidi ya watu milioni 5 wanaoishi kwa hofu ya makombora kila uchao, watoto wanaokosa fursa ya elimu kwa sababu ya hali ya usalama na pia ukosefu wa huduma ya afya kwa mamilioni ya watu ambako kuna ongezeko la magonjwa ya kifua kikuu na VVU.

Amehitimisha akisema Umoja wa Mataifa kwa upande wake unabakia na nia ya kusaidia kutafuta ufumbuzi wa amani ya kudumu na uhuru kamilifu wa taifa la Ukraine kwa mujibu wa Baraza la Usalama .