Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na Benki ya Dunia waunda bodi kudhibiti milipuko ya magonjwa

Picha ya maktaba inamwonesha mtoto kutoka Mtendera Zambia akipewa chanjo ya kipindupindu.
Picha ya Gavi Alliance/Duncan Graham-Rowe
Picha ya maktaba inamwonesha mtoto kutoka Mtendera Zambia akipewa chanjo ya kipindupindu.

WHO na Benki ya Dunia waunda bodi kudhibiti milipuko ya magonjwa

Msaada wa Kibinadamu

 

Shirika la Afya ulimwenguni WHO na Benki ya dunia wameunganisha jitihada zao na kuunda bodi itakayosaidia kuimarisha usalama wa afya duniani.

Bodi hiyo itakayoongozwa kwa pamoja na aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Gro Harlem Brundtland na Katibu Mkuu wa shirikisho la vyama vya msalaba mwekundu duniani, ICRC,  Elhadj As Sy,  itakuwa na jukumu la kufuatilia mara kwa mara mwelekeo wa magonjwa kama njia ya kuepusha kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko na ya dharura .

Uzinduzi huo umefanyika leo huko Geneva, Uswisi na kushuhudiwa na wabunifu wa mpango huo ambao ni  Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus na Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim kando mwa mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la WHO.

Dkt. Ghebreyesus amezungumzia umuhimu wa kuwa na bodi hiyo akitoa mfano wa magonjwa ya mlipuko kama Ebola nchini Jamhuri ya kidemokasia ya Congo, DRC, ambako WHO  na washirika wamekuwa wakisaidia kukabiliana nao.

Amesema mfumo waliokubaliana utafanya kazi ya kuratibu na pia  kujiandaa mapema kwa kuhakikisha wahusika wako tayari kukabiliana na milipuko hiyo na hivyo kuokoa maisha ya wengi.

Naye Dkt. Kim amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakichukua hatua za dharura kushughulikia milipuko na wakishakamilisha wanasahau kufuatialia.

Hivyo amesema mfumo walioanzisha utasaidia ufuatiliaji na pia kuandaa mazingira ya tahadhari ya mapema ili kuepusha kuzuka tena kwa magonjwa ya milipuko siku za usoni.