Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madhara ya ukimwi yagharimu mabilioni ya fedha- ILO

Monica ambaye ni mwathirika wa VVU  akiwa amemkumbatia  mjuku wake katika kijiji cha Makuzeze Zimbabwe
Picha ya UNICEF/G. Pirozzi
Monica ambaye ni mwathirika wa VVU akiwa amemkumbatia mjuku wake katika kijiji cha Makuzeze Zimbabwe

Madhara ya ukimwi yagharimu mabilioni ya fedha- ILO

Msaada wa Kibinadamu

 

Ugonjwa wa Ukimwi pamoja na kusababisha machungu kwa binadamu, pia husababisha kupotea kwa mabilioni ya mapato ya fedha kutokana na vifo vya mamia ya maelfu ya wafanyakazi ambavyo vinaweza kuzuilika kwa matibabu.

 

Shirika la kazi duniani, ILO katika ripoti yake iliyozinduliwa leo huko Geneva, Uswisi, limesema ingawa kiwango cha fedha zinazopotea kimepungua na kufikia dola bilioni 17 mwaka 2005, bado kinatarajiwa kuwa dola bilioni 7.2 mwaka 2020.

Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Guy Rider akinukuu ripoti hiyo amesema hata idadi ya wafanyakazi watakaofariki dunia kutokana na VVU na Ukimwi ifikapo mwaka 2020 inakadiriwa kupungua na kufikia 425,000 kutoka milioni 1.3 mwaka 2005.

Hata hivyo amesema vifo hivyo vinaweza kuepukika iwapo kinga na elimu vitatolewa mapema kwa waathirika na wafanyakazi wote.

Hata hivyo amesema habari njema ni  kwamba harakati za kupambana na VVU zimezaa matunda kwa kuwa wafanyakazi wanaoishi na VVU na Ukimwi wana fursa ya kuendelea kufanya kazi japo idadi yao walioko katika soko la ajira imepungua  kwa kiwango cha asilimia 83 kwa wanaume na asilimia 93 kwa wanawake.

Ripoti hiyo inapendekeza umuhimu wa kuunganisha takwimu za kiafya za kijamii na kiuchumi ili kupata takwimu sahihi za vipimo vyote vya magonjwa yanayohusiana na UKIMWI.

Ripoti hiyo pia hii imelenga  kutoa kipaumbele kwa ILO na wadau wengine katika ukusanyaji wa takwimu ili kutoa  sera na mipango ya kitaifa ya VVU na UKIMWI katika ulimwengu wa ajira.