Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Priyanka apaza sauti za watoto warohingya

Wanawake na watoto wasubiri msaada wa kibinadamu Cox's Bazar, Bangladesh, ambapo milioni moja ya wakimbizi wa Rohingya wamehifadhiwa.
Olivia Headon/IOM
Wanawake na watoto wasubiri msaada wa kibinadamu Cox's Bazar, Bangladesh, ambapo milioni moja ya wakimbizi wa Rohingya wamehifadhiwa.

Priyanka apaza sauti za watoto warohingya

Amani na Usalama

Balozi mwema wa UNICEF, Priyanka Chopra amezuru kambi ya wakimbizi wa Rohingya huko Bangladesh na kutoa wito kwa usaidizi zaidi kwa watoto wa wakimbizi hao ambao maisha yao yako taabani.

Eneo la Cox’s Bazar, nchini Bangladesh, kimbilio la wakimbizi wa Rohingya kutoka Mynmar. Taswira ya eneo hilo ni vibanda vilivyoko milimani ambapo hivi sasa ujenzi unaendelea kuelekea msimu wa pepo za monsuni.

Makazi ni duni, watoto nao mustakhbali wao ni mashakani. Maji safi na salama ni shida,  elimu nayo wanaipata kwa shida.

Ujio wa balozi mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Priyanka Chopra, waonekana kuleta matumaini, kwani atapaza sauti zao.

Chopra katika ziara yake ya siku nne kambini hapa ametembelea watoto waliokuwa darasani na kukagua kile wanachoandika na kuchora na hatimaye alicheza nao.

Kisha alizungumza na wazazi wao na kusikia machungu yao ambapo yaelezwa kuwa asilimia karibu 60 ya wakazi wakimbizi zaidi ya Laki Saba kwenye eneo hili ni watoto.

Chopra alitiwa matumaini na kazi ya UNICEF katika kuboresha maisha ya watoto ikiwemo kuhakikisha watoto wanakuwa watoto na pia wanapata lishe bora.

Na ndipo akafunguka, 'UNICEF itasaidia watoto wakati wapo hapa na kuhakikisha kuwa wanapata elimu, ili wanapokua watu wazima wahakikishe kuwa hakuna mtu ambaye anawatendea tofauti watu tofauti.”