Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhai wa nyuki ni ustawi wa binadamu- FAO

Ufugaji wa nyuki
UNMISS/Eric Kanalstein
Ufugaji wa nyuki

Uhai wa nyuki ni ustawi wa binadamu- FAO

Ukuaji wa Kiuchumi

Kuelekea siku ya nyuki duniani tarehe 20 mwezi huu wa Mei, shirika la chakula na kilimo duniani, FAO linataka hatua zaidi za kulinda nyuki ambao wana jukumu kubwa la kuchavusha maua yanayozalisha chakula.

FAO linasema zaidi ya asilimia 75 ya chakula kinachozalishwa duniani kinategemea wadudu wachavushaji maua kama vile nyuki, popo na vipepeo, hata hivyo uwepo wao duniani uko hatarini.

Mathalani FAO imesema shughuli za kilimo pamoja na matumizi ya madawa ya kuulia wadudu zinatowesha nyuki kwa hiyo imetaja mambo sita ya kuzingatia ili kuhakikisha wadudu hao adhimu wanaendelea kuwepo kama njia ya kuhakikisha upatikanaji wa chakula na kutokomeza njaa duniain.

Mambo hayo ni pamoja na kuboresha mlo wa binadamu kwa kupanda aina mbalimbali za mazao ya chakula ambayo pia ni chakula cha nyuki kama vile matunda na buni.

Hatua nyingine watu watumie asali ghafi na mazao yatokanayo na asali na hivyo kuongeza kipato cha warina asali na uzalishaji utaongezeka na kuhakikisha uwepo wa nyuki.

Halikadhalika kuwajengea nyuki wachavushaji eneo la kupata maji baada ya safari ya kutembelea maua 7,000 kila siku. FAO inasema kilo moja ya asali huzalishwa baada ya nyuki kutembelea maua milioni 4.

Shirika hilo linasema kwa kuchukua hatua hizo na hatua nyingine zilizochapishwa kwenye wavuti wake, wakazi wa dunia watasaidia kusongesha safari ya nyukia ya kuchavusha maua kwa faida siyo tu ya uhai wa nyuki bali pia lishe bora na ustawi wa kiuchumi duniani.