Wa Iraki jitokezeni kwa wingi kuwachagua viongozi wenu: Kubis
Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, Jan Kubis, yupo ziarani leo katika jimbo la Anbar, kwenye mji wa Fallujah nchini humo kushuhudia mchakato wa uchaguzi wa viongozi katika ngazi mbalimbali.
Bwana Kubis ametoa wito kwa wananchi wote wa Iraq kwenye mji wa Felluja ulioko magharibi mwa Bagdad kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo, ili waweze kuchagua viongozi watakaowaleta maendeleo katika jimbo hilo ambalo lilikombolewa na vyombo vya usalama vya Iraq kutoka kwa wanamgambo wa Isis mwaka 2016.
Viongozi wengine wa Umoja wa Mataifa walioshuhudia zoezi la Uchaguzi nchini humo ni pamoja na Alice Walpole ambaye ni mwakilishi wa Katibu Mkuu nchini Iraq katika masuala ya siasa na uchaguzi, ambaye alitembelea kambi za wakimbizi wa ndani za Kirkuk zilizopo chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa ili kujionea zoezi la uchaguzi wa viongozi katika ngazi mbalimbali.
Umoja wa Mataifa umekuwa mstari wa mbele katika kutoa msaada wa hali na mali ili kufanikisha zoezi la uchaguzi wa viongozi katika ngazi mbalimbali kama vile wabunge na wakuu wa majimbo kwa ushirikiano na tume ya uchaguzi nchini Iraq NEC.