Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watoto laki 7 wanakabiliwa na utapiamlo Kasai DRC: UNICEF

Mmoja ya watoto waliyoathirika na utapiamlo jimbo  la Kasai DRC
Picha ya UNICEF/UN064921/
Mmoja ya watoto waliyoathirika na utapiamlo jimbo la Kasai DRC

Zaidi ya watoto laki 7 wanakabiliwa na utapiamlo Kasai DRC: UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa  la kuhudumia watoto UNICEF limezindua ripoti maalum iitwayo tahadhari kuhusu  janga la utapiamlo linalowakumba watoto wenye umri wa chini ya miaka mitato huko Kasai Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

Hapa ni katika moja ya hospitali kwenye jimbo la Kasai huko DR Congo, mtoto akifanyiwa vipimo vya kiafya akionekana dhahiri kuwa ni mdhoofu kiafya.

Mtoto huyu ni miongoni mwa zaidi ya watoto laki 770 wanaokabiliwa na utapiamlo jimboni humo kutokana na ukosefu wa lishe bora, chakula kunakosababishwa na migogoro ya kikabila inayoendelea nchini humo tangu mwaka 2016.

UNICEF inasema zaidi  ya watu milioni 3.8 wana uhitaji mkubwa wa misaada ya kibinadamu ikiwemo watoto milioni 2.3.

Msemaji wa UNICEF Christophe Boulierac  ambaye alikuwa ziarani  huko Kasai,   amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kuwa

Sauti ya Christophe Boulierac

“Tunakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mahitaji muhimu kwa  mtoto katika jimbo la Kasai baada ya migogoro ya kivita iliyodumu kwa miezi 18 sasa. Jamii ya kimataifa inatakiwa  kuingilia kati tatizo hili haraka ikwezekanavyo ili kuokoa maisha ya maelfu ya watoto . Madhara ya mgogoro wa kivita huko kasai ni wa kutisha sana ambapo watoto wengi wamekuwa wakitumiwa na waasi katika kupiga vita vikosi vya serikali.

Henry Ndumbi Badianga ni mhudumu wa afya huko jimboni Kasai ambaye amekuwa mstari wa mbele kujitolea katika  kuisaidia jamii yake licha ya uwezo mdogo na ukosefu wa vitendea kazi.

Sauti Henry Ndumbi Badianga

“Nimejitolea kufanya kazi ya kuhudumia jamii hii, kwasababu nimeona watoto wengi wakiteseka na hakuna mtu wa kuwasaidia hata kuwapeleka katika vituo vya afya. Kazi ya yangu ya kwanza ni pale nilipompeleka hospitalini mtoto aliyekuwa anaumwa katika familia yangu. Baada ya hapo wahudumu wa hospitali waliniomba niweze kuwasaidia  kuwapeleka watoto wengine kwenye vituo vya afya.”