Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahisani saidieni wenye njaa Afrika Magharibi- UN

Msichana kutoka  Nigeria akitabasamu wakati wa mgao wa chakula kutoka  kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa
Picha ya WFP/Tom Saater
Msichana kutoka Nigeria akitabasamu wakati wa mgao wa chakula kutoka kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa

Wahisani saidieni wenye njaa Afrika Magharibi- UN

Msaada wa Kibinadamu

Ripoti ya  mashirika  ya  Umoja wa Mataifa inasema ukame katika ukanda wa Sahel barani Afrika  umesababisha ukosefu wa chakula kwa zaidi ya watu milioni 5,huku watoto zaidi ya milioni 1.6 wakikabiliwa na utapiamlo.

Ripoti hiyo imesema kuwa ukame uliosababishwa na ukosefu wa mvua,mfumuko wa bei na migogoro ya kivita katika baadhi ya nchi za Afrika magharibi kama Mauritania, Kaskazini mwa Senegal, Mali, Niger Burkina Faso na Chad mwaka jana vimesababisha  ukosefu  mkubwa wa chakula .

Mashirika hayo  likiwemo la chakula na kilimo duniani FAO , la watoto UNICEF na mpango wa chakula duniani WFP yamesema kupitia ripoti hiyo kwamba msaada unahitajika haraka iwezekanavyo ili kuokoa maisha ya mamilioni ya raia katika ukanda huo.

Abdou Dieng ambaye ni Mkurugenzi wa WFP kanda ya Afrika magharibi na kati amesema wamepata taarifa kuwa, kutokana na janga hilo la njaa, baadhi ya raia wamepunguza milo yao kwa siku huku  wanafunzi wakitoroka shule kutokana na ukosefu wa  chakula

UNICEF, FAO NA WFP, waliunda kikosi kazi ili kuweza kukabiliana na matatizo ya dharura yanayowababili raia katika nchi zilizoko ukanda wa Sahel, huku wakikaribisha misaada mbalimbali kutoka kwa wahisani ili waweze kusaidia mipango ya muda mrefu.

Kupitia ripoti hiyo kila shirika limetaja kiwango cha fedha inachohitaji kwa operesheni zake ambapo  WFP  inahitaji dola milioni 284 , UNICEF dola milioni 264 na FAO dola milioni 128 ili kuweza kuwafikia wahitaji laki 9 katika nchi hizo za Afrika maghribi.