Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nilichoshuhudia kinakatisha tamaa- Shearer

Mkimbizi wa ndani Sudan Kusini akiwa na virago vyake kufuatia ghasia zinazoendelea nchini humo. UNMISS (Maktaba)
UNMISS (Maktaba)
Mkimbizi wa ndani Sudan Kusini akiwa na virago vyake kufuatia ghasia zinazoendelea nchini humo. UNMISS (Maktaba)

Nilichoshuhudia kinakatisha tamaa- Shearer

Amani na Usalama

Kufuatia mapigano ya hivi karibuni huko Sudan Kusini yaliyosababisha maelfu ya watu kukimbia makazi yao, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo David Shearer amezuru maeneo hayo na kushuhudia hali halisi ikiwemo mtoto aliyenusurika kifo baada ya kupigwa risasi.

Ziara hiyo ya Bwana Shearer na ujumbe imefanyika katika jimbo la Unity ambako walikwenda kwa ndege na kufika eneo la Dablual lililo chini ya upinzani.

Alishuhudia uharibifu mkubwa na uporaji katika moja ya hospital kwenye eneo hilo pamoja na mtoto aliyejeruhiwa kwa risasi. Bwana Shearer akasema.

(Sauti ya David Shearer)

 “Kuongezeka kwa mapigano kumekuwa na madhara makubwa. Mtoto mdogo wa kike amepigwa risasi ambaye imeingia tumboni na kutokea mgongoni. Tunashukuru yuko salama. Lakini huu ni mfano wa matukio mengi kama siyo mamia hata maelfu ya watu wanaokimbia kusaka hifadhi wakiishi kwa kula majani pori na matunda ili waweze kuepuka mzozo.”


Bwana Shearer ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS hatimaye alizungumza na viongozi wa eneo hilo la Dablual waliomweleza kuwa wana hamu kubwa ya kuwa na amani na ndipo akasema.

(Sauti ya David Shearer)

“Wakati Fulani mwaka jana nilihisi tulikuwa kwenye mwelekeo mzuri. Leo baada ya hiki nilichoshuhudia,  hali inakatisha tamaa. Kwa hiyo kazi yetu ni kulinda raia na kusaidia waondokane na giza hili ili mchakato wa Amani uweze kufanya kazi na tunaweza kupata njia za kuwa na suluhu ya kudumu.”