Uchunguzi waendelea wa vifo vya watu 45 nchini Yemen

Image

Uchunguzi waendelea wa vifo vya watu 45 nchini Yemen

Amani na Usalama

“Ofisi yetu bado inajitahidi kukusanya taarifa kuhusu majina, umri na jinsia ya raia waliouawa na kujeruhiwa wakati wa tukio hilo la kikatili." Asema Liz Throssel wa Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa unaendelea na uchunguzi kubaini utambulisho wa wahanga wa mashambulizi ya anga yaliyofanyika siku nne zilizopita nchini Yemen na kusababisha vifo vya watu 45. John Kibego na ripoti kamili.

Kwa mujibu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa waliouawa ni pamoja na wanawake na watoto, huku mamia wengine wakiwa wamejeruhiwa.

Katika shambulio la kwanza la anga muungano unaoongozwa na Saudi Arabia ulishambulia basi la abiria karibu na Kijiji cha Al-Areish wilaya ya Mawza jimboni Taiz na kuua watu 21 wakiwemo watoto watano. 

Liz Throssell ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Geneva, Uswisi.

(SAUTI YA LIZ THROSSELL)

 “Watu walioshuhudia wanasema watu hao walikuwa wanarejea nyumbani kupitia barabara ndogo ya kijijini kombora la anga liliposambaratisha gari lao. Miili ya wahanga wa tukio hilo iliungua vibaya kiasi kwamba ni vigumu kuitambua.”

Shambulio la pili lilitokea Jumapili na kujeruhi watu wengi na la kusikitisha zaidi ni lile la kwenye sherehe ya harusi Jumatatu jimboni Haijah lililokatili maisha ya raia 19 na kujeruhi wengine 50. 

Ofisi ya haki za binadamu imeutaka muungano unaoongozwa na Saudia Arabia kufanya uchunguzi huru, wa kina na wa wazi wa mauaji yote hayo ya karibuni. 

Tangu kuanza kwa machafuko Yemen Machi 2015 raia zaidi ya 6,300 wameuawa na 9,900 wamejeruhiwa.