Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yamlilia mwakilishi wa Côte d’Ivoire

Bendera ya UN
UN/maktaba
Bendera ya UN

UN yamlilia mwakilishi wa Côte d’Ivoire

Amani na Usalama

Mwakilishi wa Côte d’Ivoire kwenye Umoja wa Mataifa Bernard Tanoh-Boutchoue amefariki dunia jijini New York, Marekani.

Balozi Tanoh-Boutchoue amefariki dunia jana jumatano ikiwa ni miezi michache tangu ateuliwe kushika wadhifa huo wa kuwakilisha nchi yake kwenye Umoja wa Mataifa.

Yaripotiwa aliugua Jumanne na kupelekwa hospitali na mauti kumkuta Jumatano.

Umoja wa Mataifa umepokea kwa mshtuko mkubwa kifo cha Balozi huyo ambapo Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema alikuwa na mchango mkubwa katika kusongesha jitihada za umoja huo za amani na usalama siyo tu barani Afrika bali pia duniani kwa ujumla.

Nao wajumbe wa Baraza la Usalama wameeleza masikitiko yao ambapo kabla ya kuanza kwa kikao chao leo alhamisi walisimama kwa dakika moja kumkumbuka Balozi Tanoh-Boutchoue ambaye nchi yake ni mjumbe wa Baraza hilo kwa mwaka huu.

Balozi Tanoh-Boutchoue amehudumia nchi yake katika medani ya diplomasia kwa zaidi ya miaka 40 ambapo Umoja wa Mataifa umetuma salamu za rambirambi kwa familia yake, wananchi na serikali ya Côte d’Ivoire.