Saidieni wafugaji Somalia mifugo yafa na ukame-FAO

21 Machi 2018

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limeonya leo kuwa hali ya wafugaji Somalia ni hoi  bin taaban kutokana  na ukame unaokumba eneo hilo.

Kutokana na hali hiyo FAO inasema msaada wa haraka unahitajika kwa wafugaji hao kwani utabiri wa hali ya hewa unaonyesha kuwa kipindi cha kuanzia mwezi Aprili hadi Juni mvua zitakuwa chini ya wastani.

Mkuu wa ofisi ya FAO nchini Somalia, Daniele Donati, amesema uchumi wa Somalia kawaida ni mseto wa kilimo na ufugaji na kufa kwa mifugo mingi kumeathiri vibaya watu na uchumi wa nchi hiyo.

Ameongeza kuwa ni muhimu  kuendelea kusaidia wafugaji kutokana na hasara hiyo wanayopata pamoja na kutoa chanjo na chakula kwa mifugo iliyosalia.

Taarifa ya FAO ya mfumo wa tahadhari ya mapema GIEWS, inaonyesha kuwa mifugo mingi nchini Somalia inakufa hali inayotishia hali ya chakula nchini humo.

Inaonya kuwa hali ni mbaya katika maeneo ya ufugaji ya kati na kaskazini mwa nchi hiyo.

FAO inahitaji dola milioni 236 kusaidia   wasomali takribani milioni 2.7 wa mashambani , wafugaji na wakulima ili wapate mavuno bora.

Mwaka jana FAO ilisaidia mifugo zaidi ya milioni 38 na kugawa chakula kwa mifugo 900,000 huki ikitoa lita za maji milioni 53.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter