Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yachukua hatua kukabili njaa huko Kasai, DRC

Wakimbizi wa ndani DR Congo waliopoteza makazi yao Kasai wapanga foleni kupokea chakula cha msaada huko Idiofa, mkoani Kwilu.
UNHCR/John Wesseles
Wakimbizi wa ndani DR Congo waliopoteza makazi yao Kasai wapanga foleni kupokea chakula cha msaada huko Idiofa, mkoani Kwilu.

WFP yachukua hatua kukabili njaa huko Kasai, DRC

Msaada wa Kibinadamu

Ghasia zikishamiri huko jimbo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na ufikishaji misaada nao ukigonga mwamba, shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limeibuka na mbinu mpya za kukabili njaa. 

WFP inasema imeamua kupatia kipaumbele mikakati miwili ya operesheni zake za dharura  huko Kasai.

Hatua hizo ni mgao wa fedha na usaidizi wa kitaalamu kwa wanawake na watoto ili kuepusha utapiamlo uliokithiri.

Mathalani mpango wa utoaji fedha ulianza wiki iliyopita ambapo wanufaika wanapatiwa dola 15 kila mmoja kwa mwezi ili kununua atakacho kwenye eneo lao.

Hadi sasa watu 38,000 wamenufaika na mpango ni kuongeza maradufu idadi hiyo katika wiki chache zijazo.

Kwa upande wa lishe, WFO imepatia watoto 56, 000 vyakule vyenye virutubisho ikiwa ni ongezeko kutoka watoto 21,000 waliopatiwa huduma hizo miezi mitatu ya mwisho ya mwaka jana.

Mwakilishi wa WFP nchini DRC Claude Jibidar amesema mpango wa lishe na fedha unaokoa maisha haraka akisema hata hivyo bado hawajaweza kutoa usaidizi wanaotaka kutokana na ukata na vikwazo vya kiusalama.

Tathmini inaonyesha kuwa watu milioni 3.2 wengi wao wakiwa ni wakulima wanakabiliwa na uhaba wa chakula huko Kasai.