Skip to main content

MINUSCA yalaani vikali kuuawa kwa mlinda amani Bangui

MINUSCA yalaani vikali kuuawa kwa mlinda amani Bangui

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA, umelaani vikali kuuawa kwa mlinda amani mjini Bangui, mnamo Juni 24.

Kwa mujibu wa taarifa ya MINUSCA, mlinda amani huyo aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana, na baadaye mwili wake kupatikana kwenye hospitali kuu ya Bangui katika mazingira tatanishi.

Kwa mujibu wa Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa MINUSCA, Parfait Onanga-Anyanga, uchunguzi unafanyika kukusanya ushahidi kuhusu kitendo hicho cha uhalifu, na kwamba kila liwezekanalo litafanywa ili kuwafikisha waliotekeleza mauaji hayo mbele ya sheria.

MINUSCA imetuma risala za rambirambi kwa familia ya mhanga, na kwa nchi yake.