Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Patricia Espinosa kumrithi Figueres UNFCCC:Ban

Patricia Espinosa kumrithi Figueres UNFCCC:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo amemteua Bi Patricia Espinosa Cantellano wa Mexico kama katibu mkuu mtendaji wa mkataba wa Umoja wa mataifa wa mabadiliko ya tabia nchi (UNFCCC).

Uteuzi huo umefanyika baada ya majadiliano na pande zote husika. Bi Espinosa atachukua nafasi ya Christiana Figueres wa Costa Rica ambaye Katibu Mkuu amemshukuru saana kwa msaada na mchango wake mkubwa katika kurejesha Imani katika majadiliano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, kufanikiwa kuimarisha ushirikiano baina ya serikali na sekta zote katika jamii katika kusukuma mbele mipango na hatua za mabadiliko ya tabia nchi .

Pia amempongeza kwa jukumu muhimu, uongozi bora na kujitolea kwake kumuunga mkono Katibu Mkuu , mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa, na wadau wote UNFCCC katika kufanikisha makubaliano ya kihistoria ya kimataifa ya Paris 2015 kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Hivi sasa Bi Espinosa ni balozi wa Mexico Ujerumani tangu mwaka 2013 na kabla ya hapo alikuwa waziri wa mambo ya nje wa Mexico tangu 2006 hadi 2012. Anakuja na ujuzi wa miaka zaidi ya 30 katika uhusiano wa kimataifa, uliojikita hususani katika mabadiliko ya tabia nchi, uongozi wa kimataifa, maendeleo endelevu, usawa wa kijinsia na ukulinda haki za binadamu. Amezaliwa mwaka 1958, ana shahada ya uzamili katika sheria za kimataifa, na shahada yake ya kwanza ni kuhusu uhusiano wa kimataifa.