Zaidi ya watoto nusu milioni wameathiriwa na mzozo Ukraine- UNICEF
Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF, limesema kuwa watoto zaidi ya nusu milioni wameathiriwa na miaka miwili ya mzozo nchini Ukraine, zaidi ya laki mbili kati yao wakihitaji usaidizi wa kisaikolojia na kijamii.
Watoto walioathiriwa zaidi ni wale wanaoishi katika maeneo yasiyodhibitiwa na serikali mashariki mwa nchi hiyo, na wale walio kwenye maeneo yaliyo mstari wa mbele katika mapigano.
Mwakilishi wa UNICEF nchini Ukraine, Giovanna Barberis, amesema miaka miwili ya machafuko, mashambulizi ya mabomu na uoga, imeacha kovu lisilofutika kwa maelfu ya watoto nchini humo.
Amesema mzozo huo unapoendelea kutokota, watoto hao wanapaswa kufikiwa hima ili kukidhi mahitaji yao ya kimwili na kisaikolojia. Zaidi ya watoto 215,000 wamefurushwa makwao kutoka maeneo yaliyoathiriwa na mzozo.