Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Brazil yakumbushwa isibinye haki za binadamu inapojiendeleza kiuchumi

Brazil yakumbushwa isibinye haki za binadamu inapojiendeleza kiuchumi

Kikundi kazi cha Umoja wa Mataifa kuhusu biashara na haki za binadamu, kimeihimiza Brazil kufanya juhudi zaidi kufanya maendeleo ya kiuchumi kwa njia inayoheshimu haki za binadamu, kufuatia ziara ya siku kumi nchini humo.

Mtaalam wa haki za binadamu, Pavel Sulyandziga, ambaye alikuwa mmoja wa ujumbe huo, ameihimiza nchi hiyo iondokane na mfumo wa kupanga na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo bila kushauriana na jamii zinazoathiriwa na miradi hiyo, zikiwemo za watu wa asili.

Katika ziara hiyo, kikundi kazi hicho kilikuta kuwa wiki sita baada ya bwawa la Fundão kuvunjika na kusababisha janga kubwa la kimazingira na athari mbaya kijamii, mabwawa mengine kadhaa bado yamo katika hatari ya kuvunjika.

Aidha, wamesema kwamba mapendekezo ya marekebisho katika kanuni za uchimbaji migodi yanaendeleza hali ya hatari kwa mazingira na jamii, huku watetezi wa haki za binadamu na watu wa asili wakiendelea kukabiliwa na vitisho kwa uhai na ardhi yao.