Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon alaani mashambulizi ya kigaidi Nigeria

Ban Ki-moon alaani mashambulizi ya kigaidi Nigeria

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesikitishwa sana na ripoti kuhusu mamia ya watu waliokufa wiki iliyopita kwenye maeneo ya Baga, katika jimbo la Borno, nchini Nigeria, karibu na mpaka wa Chad.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wake, hali ya usalama nchini Nigeria na kwenye ukanda huo bado iko kwenye nafasi ya juu katika ajenda ya Katibu Mkuu.

Jumamosi hii, msichana wa miaka 10 ameripotiwa kujilipua na bomu katika soko la Maidugiri, katika jimbo la Borno, ambapo watu takriban 19 wamekufa kwenye tukio hilo.

Katibu mkuu amelaani vikali tukio hilo linalodaiwa kutekelezwa na kundi la wagaidi la Boko Haram.

Aidha ameeleza kwamba Umoja wa Mataifa u tayari kusaidia serikali ya Nigeria na nchi jirani zilizoathirika na mzozo ili kusitisha uhalifu na kupunguza mateso ya raia.