Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalam wa UM wahofia hatma ya wafungwa wa Guantánamo

Wataalam wa UM wahofia hatma ya wafungwa wa Guantánamo

Wataalamu maalumu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameelezea kushangazwa na kuhamishwa kwa Djamel Ameziane kutoka Guantánamo Bay kwenda Algeria, huku wakitaja kuhofia hatma ya wafungwa wanaoshukiwa kushiriki ugaidi katika gereza hilo la Guantánamo Bay.

Wataalamu hao, Juan E. Méndez anayehusika na utesaji na Ben Emmerson anayehusika na haki za binadamu na vita dhidi ya ugaidi wamesema wanahofia usalama wa Bwana Ameziane akiwa Algeria, huku wakitaja mifano ya zamani ya watu walorejeshwa kwa lazima kwa nchi zenye historia na sifa ya utesaji, na ambako watu huzuiliwa kwa muda mrefu, bila mawasiliano yoyote.

Huku wakizingatia kuwa serikali ya Marekani imeomba na kupewa hakikisho na serikali ya Algeria ya kwamba Bwana Ameziane hatoteswa, wataalam hao wamesema ahadi za kidiplomasia haziwezi kutegemewa katika kutoa ulinzi dhidi ya utesaji na kutendewa maovu, na kwamba serikali zisikubali kutegemea ahadi kama hizo.