Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi wa ukombozi wa Afrika: Mwakilishi wa AU

14 Oktoba 2013

Mwangalizi wa Kudumu wa Muungano wa Nchi za Afrika kwenye UMoja wa Mataifa, Antonio Tete, amemtaja Hayati Mwalimu Julius Nyerere kama mtu anayekumbukwa kama kiongozi wa ukombozi wa Afrika.

Akiongea wakati wa kuadhimisha Siku ya Mwalimu Julius Nyerere, ambayo imeadhimishwa kwa mara ya kwanza kwenye Umoja wa Mataifa, Bwana Tete amemsifu Mwalimu Nyerere kama kiongozi mwenye uadilifu, ujasiri na shujaa wa uhuru wa Afrika.

“Kama kiongozi mwenye busara, Mwalimu alichangia sana katika mjadala kuhusu pengo la maendeleo ya kiuchumi baina ya mataifa ya Kaskazini na yale ya Kusini mwa dunia. Hafla ya leo ni muhimu kwa sababu inaenda sambamba na maadhimisho ya uzinduzi wa Umoja wa Afrika, ambao Mwalimu alichangia sasa kama mmoja wa waanzilishi wake.”

Ameongeza kuwa Mwalimu Nyerere alipigania uhuru wa nchi za Afrika na haki ya kijamii. Alikuwa kielelezo cha uongozi kwa nchi zote za Afrika katika mapambano yao ya uhuru na hamu ya amani, uhuru na maendeleo ya kiuchumi.”