Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili uimarishaji wa amani Afrika Magharibi na hali CAR

Baraza la Usalama lajadili uimarishaji wa amani Afrika Magharibi na hali CAR

Hapa New York hii leo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limekutana kujadili suala la uimarishaji wa amani katika eneo la Afrika Magharibi, pamoja na hali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Joshua Mmali ameufuatilia mkutano huo.

(Taarifa ya Joshua)

Mkutano wa leo wa Baraza la Usalama umeanza kwa wanachama kurithia taarifa ya rais wa Baraza hilo kuhusu uharamia katika ukanda wa Afrika Magharibi.

Kuhusu hali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu, na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Babacar Gaye, ameliambia Baraza hilo katika ripoti ya Katibu Mkuu kuwa ingawa taasisi za mpito zimewekwa, bado hakuna utaratibu wa kisheria nchini humo kwa ujumla, ingawa hali imetengamaa kidogo katika mji mkuu, Bangui.

 (SAUTI YA BABACAR GAYE)

Uporaji wa mali za watu, wizi, utekaji nyara, utesaji na mauaji yanaendelea. Ukiukwaji wa haki za binadamu umeenea, ukichangiwa hasa na kusambaratika kwa utaratibu wa kisheria, hususan mikoani ambako wafuasi wa Seleka wamaendelea kuwanyanyasa raia. Ni lazima tuhakikishe kuwa hakuna ukwepaji wa mkono wa sheria kwa wakiukaji wakubwa wa haki za binadamu.

Bwana gaye amesema hali ya kibinadamu imezidi kuzorota kwa kiwango kikubwa tangu mwezi Disemba 2012, na kuwa hali kanganishi ya dharura- ujumbe ambao umesisitizwa katika hotuba ya Mratibu Mkuu wa Misaada ya Kibinadamu katika Umoja wa Mataifa, Valerie Amos, kwa Baraza la Usalama, kufuatia ziara yake nchini humo Julai 11 hadi 12.

(SAUTI YA VALERIE  AMOS)