Ban ameteua Kay kumwakilisha huko Somalia, anachukua nafasi ya Balozi Mahiga

29 Aprili 2013

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amemteaua Nicholas Kay wa Uingereza kuwa mwakilishi wake maalum huko Somalia, akichukua nafasi ya Balozi Augustine Mahiga kutoka Tanzania anayemaliza muda wake mwezi Juni mwaka huu.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nersiky amemkariri Bwana Ban akimpongeza Balozi Mahiga kwa uongozi wake wa mfano na wa kujituma katika kipindi cha miaka mitatu uliowezesha kuhitimishwa kwa kipindi cha mpito wa kisiasa nchini Somalia.

Amesema mchango wa Balozi wa Mahiga umeweka msingi ambao serikali ya Somalia kwa msaada wa jumuiya ya kimataifa wanaweza kujikita zaidi katika ujenzi wa amani, kuimarisha usalama na kuleta maendeleo ya nchi hiyo.

Bwana Kay kwa sasa ni mkurugenzi wa masuala ya Afrika katika ofisi ya Uingereza inayohusika na masuala ya kigeni na jumuiya ya madola.