Pillay, Falk waelezea hofu kuhusu afya ya mahabusu wa Kiapalestina

13 Februari 2013

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, ameelezea hofu yake kufuatia ripoti za kudhoofika kwa afya ya mahabusu watatu wa Kipalestina wanaozuiliwa na Israel, na ambao wanafanya mgomo wa kutokula chakula.

Tarek Qa’adan na Jafar Azzidine wamekuwa kwenye mgomo huo kwa siku 78, ili kupinga kuzuiliwa kwao na Israel, huku Samer Al-Issawi akiwa kwenye mgomo wa kutokula mara kwa mara kwa siku 200.

Bi Pillay kusikitishwa kwake na matumizi ya vifungo vya utawala  vinavyotekelezwa na Israel, akisema kuwa watu walozuiliwa ni lazima wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria na kuhukumiwa kwa kulingana na kanuni za sheria za kimataifa au waachiliwe haraka.

Naye mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa anayefuatilia masuala ya ukiukaji wa haki za Wapalestina unaodaiwa kufanywa na Israel, Richard Falk, ametoa wito mahabusu hao watatu waachiliwe mara moja, akisema kuendelea kuwazuilia ni unyama.