Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM walaani mauwaji ya kwenye makao makuu ya polisi Kirkuk

UM walaani mauwaji ya kwenye makao makuu ya polisi Kirkuk

Mwakilishi maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq amelaani vikali shambulizi la kupangwa lililolenga makao makuu ya jeshi la polisi, katika mji wa Kirkuk ulioko kaskazini mwa nchi hiyo na kuua watu kadhaa na wengine kujeruhiwa.

Martin Kobler ambaye pia anaongoza ofisi ya ujumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Iraq UNAMI amesema amepokea kwa masikitiko makubwa tukio la shambulizi hilo na dua zake sasa zipo kwa wale waliopoteza maisha.

Amesema watekelezaji wa tukio hilo ni watu waliobeba sura ya ukatilii na ambao hawathamini uhai wa binadamu.

Kobler ameutaka utawala wa Iraq kuchukua hatua mahsusi kukabiliana na matukio ya jinsi hiyo ambayo yameanza kurejea katika mji huo

Katika shambulizo hilo watu 16 walipoteza maisha wakati mtu aliyejitoa mhanga alipolipua bomu kwenye ofisi yaliyoko makao makuu ya polisi.