Hatma ya demokrasia nchini Misri iko mashakani: IPU

12 Disemba 2012

Chama cha mabunge duniani, IPU kimesema harakati za kupigania demokrasia nchini Misri hazitakuwa na ukomo bila ya kuwepo kwa katiba inayokubaliwa na wananchi wote na ambayo pia itawahakikishia haki na usawa.

Rais wa IPU Abdelwahad Radi amekaririwa akisema hayo huku akilaani matukio ya siku za karibuni ya ghasia na vifo nchini Misri na kitendo cha serikali kutumia jeshi ili kuweka utulivu.

Amesema maana halisi ya demokrasia na uongozi thabiti wa kidemokrasia ni kusikiliza na kuwakilisha sauti za watu wote na kwamba katiba inapaswa kutokana na misingi ya nchi iwapo nchi husika inataka mustakbali wake uwe wa amani.

Bwana Radi ameitaka Misri kutumia fursa ya sasa ya kipekee ya kuandaa katiba mpya kujenga nchi yenye umoja badala ya kujenga nchi kwa misingi ya tofauti za kisiasa, kidini na jinsia.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter