Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wapata ahadi ya kutowatumia watoto katika vita kutoka kwa Serikali ya Yemen na Kundi la Al Houthi

UM wapata ahadi ya kutowatumia watoto katika vita kutoka kwa Serikali ya Yemen na Kundi la Al Houthi

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto na vita vya silaha, Leila Zerrougui, amepata hakikisho kutoka kwa serikali ya muungano ya Yemen la kukomesha matumizi ya watoto katika jeshi lake.

Bi Zerougui ambaye yupo Yemen kukagua hali ya watoto waloathiriwa na mzozo, amekutana na Rais Abd Rabbo Mansour Hadi na Waziri Mkuu, Mohammed Saleh Basindwa, pamoja na kamati ya masuala ya kijeshi ya usalama na utulivu. Amekutana pia na watoto waloathiriwa na mzozo huo, wawakilishi wa bunge la watoto na wawakilishi wa mashirika ya umma. Amepata pia kusafiri hadi jimbo la Sa’ada, ambako alikutana na kiongozi wa kundi lenye silaha la Al Houthi, Abdul Malik Badraldeen Al Houthi.

Makundi manne nchini Yemen yamewekwa kwenye orodha ya aibu ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa sababu za kutumia watoto kama wanajeshi, yakiwa ni jeshi la serikali, kundi lenye silaha la Ali Mohsen, wanamgambo wa kikabila wanaoiunga serikali na kundi la Al Houthi.