IOM yaipiga jeki Papua New Guinea

9 Novemba 2012

Kisiwa cha Papua New Guinea kinatazamia kuboresha vitengo vyake vinavyohusika na uhamiaji pamoja na ustawi wa kiraia kufuatiwa kuzinduliwa kwa mpango mpya wa kitaalamu unaoratibiwa na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na uhamiaji IOM.

Kuzinduliwa kwa mpango huo kunafuatia mkutano uliofanyika juma hili ukiwakutanisha wataalamu wa ngazi za juu kutoka pande zote waliokutana katika bandari ya Moresby.

Papua New Guinea inatajwa kuwa na uchumi dhabiti uliochagizwa na shughuli za uchimbaji madini hatua ambayo inatoa msukumo wananchi wa mataifa mbalimbali kuelekea nchini humo.

Wataalamu wa mambo wanasema kuwa ukuaji wa kasi wa uchumi na kuendelea kuitengamaa mifumo ya uzalishaji mali, kunatoa changamoto katika maeneo ya uhamiaji na utunzaji wa rasilimali za umma.

IOM inasema kuwa kuanzishwa kwa mfumo mpya ambao utawajengea uwezo wa kitaalamu maafisa wa uhamiaji, kunatazamia kutoa mchango mkubwa hasa wakati huu ambapo serikali inaboresha ustawi wa raia wake.