Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azipongeza Sudan na Sudan kusini kwa kusaini mikataba kuhusu usalama na uchumi

Ban azipongeza Sudan na Sudan kusini kwa kusaini mikataba kuhusu usalama na uchumi

Mikataba ilotiwa saini kati ya serikali za Sudan na Sudan Kusini kuhusu usalama, mipaka na uhusiano wa kiuchumi ni muhimu kwa ajili ya utulivu na maendeleo ya nchi hizo mbili, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon. Kwa mujibu wa msemaji wake, Martin Nesirky, Bwana Ban ameikaribisha mikataba hiyo, ambayo imesainiwa mjini Addis Ababa, Ethiopia siku ya Alhamis.

"Katibu Mkuu amezipongeza pande zote na hasa marais Omar el-Bashir na Salvar Kiir kwa kuonyesha uongozi wa busara, ambao umewezesha mikataba hiyo kusainiwa, na kwa kuchagua amani badala ya vita. "

Mikataba hiyo imesainiwa chini ya upatanishi wa tume ya Muungano wa Afrika inayoongozwa na rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki.

Bwana Ban ameyahimiza mataifa hayo mawili kutafuta suluhu kuhusu hatma ya maeneo yanayozozaniwa, pamoja na hatma ya eneo la Abyei lenye utajiri mwingi wa mafuta. Ametoa wito kwa serikali za nchi hizo mbili zirejelee sasa utekelezaji wa mikataba hiyo, ili kukamilisha harakati walizoanzisha, na kwamba Umoja wa Mataifa u tayari kuzisaidia katika juhudi hizo, kwa ushirikiano na wadau wengine.