Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Visa 26 zaidi vyafanyiwa uchunguzi wa Ebola nchini DRC

Visa 26 zaidi vyafanyiwa uchunguzi wa Ebola nchini DRC

Kufikia tarehe 15 Septemba, visa 46 vya ugonjwa wa Ebola vilikuwa vimeripotiwa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Kati ya hivyo, 14 vilikuwa vimethibitishwa kama homa ya Ebola, na vingine 32 vikiwa vya kukisia tu. Watu 19 wamefariki dunia kufikia sasa kati ya visa vyote 46 ambavyo vimeripotiwa, lakini ni vifo sita tu kati ya vyote vilivyothibitishwa kutokana na homa ya Ebola.

Visa vyote ambayo vimeripotiwa ni kutoka kata mbili, zikiwa ni Isiro na Haut-Uélé katika wilaya ya Viadana, mkoa wa Orientale. Kuna visa vingine 26 ambavyo vimeripotiwa na vinafanyiwa uchunguzi.

Wizara ya afya nchini DRC inaendelea kushirikiana na wadau wengine, likiwemo Shirika la Afya Duniani, WHO ili kudhibiti mlipuko wa homa hiyo hatari ya Ebola. Mashirika ya WHO na shirika la kimataifa linalokabiliana na milipuko ya magonjwa hatari, GOARN, yanasaidia kwa kupeleka wataalam kushirikiana na wadau katika kuratibu, kuzuia maambukizi, kufanya uchunguzi wa maabara, kufuatilia na kutoa maelezo kwa umma.