Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yashirikiana na Mastercard kutoa misaada ya chakula wakitumia Teknolojia ya Digital

WFP yashirikiana na Mastercard kutoa misaada ya chakula wakitumia Teknolojia ya Digital

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, leo limetangaza ushirikiano wa kimataifa na Kampuni ya huduma za fedha ya MasterCard, ambao utatumia ubunifu wa digital kuwasaidia watu kote duniani kuepukana na njaa na umaskini. Ushirikiano huo utatumia utaalam wa Mastercard katika huduma za malipo ya njia ya elektroniki, na uwezo wa WFP kufika kila pembe ya dunia penye watu walio na njaa, ili kukidhi mahitaji ya lishe kwa watu walio hatarini zaidi.

Mkurugenzi wa mawasiliano, sera za umma na ushirikiano na mashirika ya kibinafsi katika WFP, Nancy Roman, amesema kuwa kampuni ya Mastarcard ni mfano wa jinsi ushirikiano na kampuni za kibinafsi unaweza kufanya ubunifu dhidi ya njaa.

Ameongeza kuwa kwa kutumia ujuzi wa kitaaluma wa Mastercard, WFP itaendeleza zaidi mfumo wake wa vocha za elektroniki, ambao unazisaidia familia zenye njaa kote ulimwenguni kununua vyakula vyenye lishe bora kutoka masoko yaliyo karibu nao, na pia kupitia mpango wake wa misaada ya tovuti inayolenga wait binafsi na makampuni katika jamii ya kimataifa inayojihusisha na kupata suluhu kwa tatizo la njaa.