Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa IAEA asikitishwa na kushindwa kwa mazungumzo na Iran

Mkuu wa IAEA asikitishwa na kushindwa kwa mazungumzo na Iran

Mkuu wa shirika la kimataifa la nguvu za atomiki la Umoja wa Mataifa, Yukiya Amano, leo ameitaka Iran kuwaruhusu wakaguzi wa shirika hilo kwenda kwenye kituo cha kijeshi cha Parchin.

Bwana Amano ameelezea kusikitishwa kwake kwamba shughuli ambazo zimekuwa zikiendelea katika kituo hicho tangu mwezi Februari zinaathiri uwezo wa IAEA kufanya ukaguzi wake wa kuhakiki ikiwa mpango wa Iran wa nyuklia ni wa amani. Iran imesema katika barua ya agosti 29 kuwa madai yanayohusiana na kituo cha Parhin hayana msingi wowote.

Bwana Amano amesema kuwa ingawa kumekuwa na mazungumzo kati ya IAEA na Iran tangu mwezi Januari, hakujakuwepo matokeo yoyote ya ufanisi, na kutaja kuwa hilo linakera, kwani bila ushirikiano wa Iran, haitawezekana kuanzisha harakati za kupata suluhu kwa masuala yote, likiwemo hofu ya kuwa huenda mpango wa Iran wa nyuklia ni kwa ajili ya vita.