Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay asikitishwa na hukumu kali dhidi ya wanaharakati wa Bahrain

Pillay asikitishwa na hukumu kali dhidi ya wanaharakati wa Bahrain

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay, amesema kwamba uamuzi wa mahakama ya rufaa ya Bahrain kuhifadhi hukumu zilizotolewa dhidi ya wanaharakati 20 wa kisiasa ni wa kusikitisha.

Bi Pillay amesema kwamba awali, alikuwa amekaribisha uamuzi wa serikali ya Bahrain kuhamishia kesi hizo kwa mahakama ya umma, kwani mahakama za kijeshi hukabiliwa na matatizo ya kuhakikisha kwamba usawa, uwazi na utekelezaji wa haki unatimizwa. Lakini sasa ameelezea kusikitishwa kwake kutokana na ukubwa wa mashtaka yaliyowakabili wanaharakati hao na ushahidi mdogo uliotolewa, na kuelezea kusikitishwa kwake kwamba mahakama ya rufaa imeshikilia uamuzi wa kutoa hukumu kali, vikiwemo vifungo vya maisha.

Awali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, alikuwa ametoa wito kwa serikali ya Bahrain kuwaruhusu washtakiwa wote kutekeleza haki yao ya kuomba rufaa, na kuhakikisha kuwa utaratibu unaofaa kisheria na kanuni za kimataifa za haki za binadamu zinafuatwa.