Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM Waipongeza Serikali ya Somalia kwa Kusaini Mkakati wa Kukomesha ajira ya watoto katika jeshi

UM Waipongeza Serikali ya Somalia kwa Kusaini Mkakati wa Kukomesha ajira ya watoto katika jeshi

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya watoto kwenye maeneo ya vita, Radhika Coomeraswamy, ameipongeza serikali ya mpito ya Somalia kwa kutia saini mkakati wa kukomesha ajira ya watoto katika jeshi. Mkakati huo umetiwa saini na waziri wa ulinzi wa Somalia ambaye pia ni naibu waziri mkuu, Hussein Arab Isse mjini Rome. Mkakati huo unaweka mwongozo wa hatua zitakazochukuliwa na serikali ya Somalia kuhakikisha kuwa jeshi lake la kitaifa halina watoto tena.

Kulingana na mkakati huo, serikali ya Somalia pia inajitolea kuhakikisha kuwa watoto wote wanaotolewa katika jeshi wanarejeshwa kwenye maisha ya kawaida, na kuweka sheria ya kitaifa ambayo itafanya ajira ya watoto katika jeshi kuwa hatia. Serikali hiyo pia itahitajika kuruhusu Umoja wa Mataifa kwenda kwa kambi za kijeshi kuhakiki kuwepo kwa watoto au la.

Ikiwa serikali ya Somalia itatimiza majukumu yake kulingana na mkakati huo, basi itaondolewa kwenye orodha ya Katibu Mkuu ya mataifa na makundi yanayowaingiza na kuwatumia watoto katika vita vya silaha. Hafla ya kuutia saini mkataba huo imefanyika kwenye mkutano wa Kundi la Kimataifa linalofuatilia masuala ya Somalia, na imeshuhudiwa na Waziri Mkuu na Spika wa bunge la mpito la Somalia. Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya Somalia, Augustine Mahiga, aliusaini mkakati huo kwa niaba ya Umoja wa Mataifa.