Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalam wa Umoja wa Mataifa ahimiza Serikali ya Azerbaijan iongeze Bajeti ya Afya

Mtaalam wa Umoja wa Mataifa ahimiza Serikali ya Azerbaijan iongeze Bajeti ya Afya

Mtaalam Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya afya, Anand Grover, ametoa wito kwa serikali ya Azerbaijan iongeze bajeti yake ya idara ya afya ili ifikie kiwango cha kimataifa. Bwana Grover amesema haya mwishoni mwa ziara yake ya siku nane nchini humo. Ameongeza kuwa kuongeza fedha zinazotumiwa katika idara ya afya ni muhimu, ili kuhakikisha kuwa utajiri mwingi ilio nao nchi hiyo unatumiwa kuboresha afya ya raia wake.

Bwana Grover, ambaye amekuwa akiizuru Azerbaijan kukagua masuala ya haki ya afya- ikiwemo kifua kikuu na huduma za afya katika magereza- amesema kuwa raia wa Azerbaijan hawastahili kupewa nafasi ya chini, na kwamba serikali ya taifa hilo ni sharti ijiulize ikiwa inawekeza ipasavyo katika afya ya watu wake ili kuhakikisha haki ya kuwa na afya nzuri kwa wote.