Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchumi utaendelea kudorora Asia-Pacific mwaka 2012:ESCAP

Uchumi utaendelea kudorora Asia-Pacific mwaka 2012:ESCAP

Eneo la Asia na Pacific linakabiliwa na mwaka mwingine wa mdororo wa uchumi huku mahitaji ya bidhaa zake za nje yakishuka kwenye mataifa yaliyoendelea na gharama za mitaji zikiongezeka. Hata hivyo eneo hilo limeelezwa kuwa litaendelea kuwa kiungo kicho cha uchumi duniani kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa yaliyotolewa mjini Bangkok na tume ya uchumi na masuala ya jamii ya Asia-Pacific ESCAP.

ESCAP inasema kiwango cha ukuaji uchumi katika mataifa yanayoendelea kinakadiriwa kupungua na kufika asilimi 6.5 mwaka huu kutoka asilimia 7.0 ya mwaka jana, au ukilinganisha na asilimia 8.9 ya mwaka 2010.

Kuyumba kwa bei ya bidhaa ni tatizo kubwa inasema ripoti ya ESCAP katika eneo hilo ambalo linakabiliwa na matatizo ya kupanda kwa bei kwa muda mrefu. Ripoti hiyo imemulika zaidi mafanikio ya eneo hilo katika wakati huu ambapo bei za bidhaa ni za juu sana dunia kote.