Ban asisitiza umuhimu wa ushirikiano wa Umoja wa Mataifa na muungano wa Afrika

13 Januari 2012

Juhudi za pamoja za Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika zimeimarisha amani na usalama katika bara hilo, amesema Katibu Mkuu Ban Ki-moon, akichangia mjadala kuhusu suala hilo katika Baraza Kuu uliopendekezwa na Afrika Kusuni.

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma aliongoza mjadala huo mjini New York jana kwa kuwa nchi yake ndio mwenyekiti wa Baraza la Usalama mwezi huu.

Bwana Ban alisema kwamba kuna haja ya kuendelea kuimarisha ushirikiano huo ili kuzuia migogoro na kuchangia katika kutafuta mapatano.

Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika yamekuwa yakifanya kazi pamoja kutafuta suluhu katika eneo la Darfur nchini Sudan na Somalia, alisema Bwana Ban. Juhudi za pamoja pia zinafanywa kukabili tisho la mashambulizi yanayotelezwa na kundi liitwalo Lord’s Resistance Army (LRA) katika mataifa kadhaa ya Afrika mashariki na ya kati, Bwana Ban amesema.

Amependekeza njia kadhaa za kuimarisha ushirikiano, zikiwemo kushirikisha mashirika yasiyo ya kiserikali na makundi ya wanawake yanayoendesha miradi ya kudumisha amani barani Afrika.

Kamishina wa amani na usalama wa Muungano wa Afrika, Ramtane Lamamra, alisema kwamba vitisho vipya kwa usalama Afrika vimezuka, kama vile ugaidi, uharamia baharini and mabadiliko ya hali ya hewa, bali na kuwa bara hilo ndilo pia lenye migogoro mingi kuliko maeneo mengine.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter