Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yalaani mauaji ya waandishi wa habari wa Ufilipino na Syria

UNESCO yalaani mauaji ya waandishi wa habari wa Ufilipino na Syria

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO leo amelaani vikali mauaji ya hivi karibuni ya waandishi wa habari Ufilipino na Syria na kuzitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina wa mauaji hayo.

Bi Bokova amesema anaitaka serikali ya Ufilipino kuchunguza kwa kina uhalifu huo na kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria, ameongeza kuwa ni muhimu vitendo kama hivyo vinavyokiuka haki za uhuru wa kujieleza kutofumbiwa macho.

Kwa mujibu wa shirika la waandishi wa habari wasio na mipaka Christopher Guarin mtangazaji wa mtandao wa Radio Mindanao na mhariri wa gazeti la Tatak News Nationwide alikuwa akirejea nyumbani na mkewe na watoto wake Alhamisi iliyopita gari lake lilipofyatuliwa risasi na mtu asiyejulikana aliyekuwa kwenye pikipiki. Christopher alijeruhiwa na alipojaribu kukimbia ndipo alipopigwa risasi tano na kufariki dunia.Na mkewe amesema ameshapata vitisho vingi vya kuuawa siku za nyuma.

Bi Bokova amelaani pia maaji ya Shoukri Ahmed Ratib Abu Borghoul wa Syria ambaye alipigwa risasi tarehe 30 Desemba mwaka jana na kufariki dunia siku tatu baadaye kutokana na majeraha. Alilengwa na kundi la watu wenye silaha alipokuwa akirejea nyumbani kwenye mji wa Darya karibu na mji mkuu Damascus baada ya kumaliza kutangaza kipindi chake cha kila wiki redioni.