Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa Baraza Kuu ahitimisha ziara ya siku moja nchini Somalia

Rais wa Baraza Kuu ahitimisha ziara ya siku moja nchini Somalia

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Nassir Abdulaziz Al-Nasser amehitimisha ziara ya sik moja nchini Somalia alikoambatana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.

Akiwa Moghadishu bwana Al-Nasser na Katibu Mkuu wamekutana na Rais wa serikali ya mpito ya Somalia Sheikh Sharif Sheikh Ahmed, waziri mkuu Adiweli Mohamed Ali na spika wa bunge la nchi hiyo Sharif Hassan Sheikh.

Viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali yakiwemo matatizo ya kibinadamu, hali ya usalama Somalia na utekelezaji wa ramani mpya aya amani ya taifa hilo lililoghubikwa na vita kwa zaidi ya miongo miwili. Katika mkutano na viongozi wa serikali ya mpito Rais wa baraza kuu Al-Nasser amerejea wito kwamba utekelezaji wa ramani ya amani iliyoidhinishwa Septemba ndio njia pekee ya kusonga mbele. Pia amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa wako tayari kutoa msaada wowote watakaoweza kili kusaidia kufanikisha utekelezaji huo.

Na alipokutana na wafanyakazi wa misaada wa kimataifa na kitaifa amepongeza kazi kubwa ya kuokoa maisha wanayoifanya na kusisitiza kuwa usalama wao ni kipaumbele cha kwanza. Ameahidi msaada wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa serikali na watu wa Somalia.