Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kesi ya kukashifu dhidi ya mwanasiasa wa upinzani Cambodia yautia hofu UM

Kesi ya kukashifu dhidi ya mwanasiasa wa upinzani Cambodia yautia hofu UM

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay amelelezea hofu yake juu ya kesi ya kumuharibia jina mtu inayoendelea dhidi ya mwanasiasa wa upinzani nchini Cambodia na kusema inatoa ishara ya kuporomoka kwa uhuru katika taifa hilo.

Mu Sochua ambaye ni mbunge nchini Cambodia , waziri wa zamani wa masuala ya wanawake na mtetezi mkubwa wa haki za wanawake , mwezi Agosti mwaka jana alikutwa na hatia ya kumuharibia jina waziri mkuu Hu Sen alipotangaza mwezi Aprili kwamba atamshitaki kwa matamshi aliyotoa ya kumshushia hadhi.

Matamshi ya waziri mkuu huyo yalikuwa ni pamoja na kuelezea kutofunga kishikizo cha blauzi ya Bi Sochua na mengine yanayohusiana na ngono ambayo yalimfanya bi Sochua kufungua mashitaka ya kuchafuliwa jina dhidi ya waziri mkuu huyo.

Hata hivyo kesi ya Bibi huyo dhidi ya waziri mkuu ilifutwa, kinga yake ya ubunge kutolewa na kasha akakutwa na hatua ya kumuharibia waziri mkuu jina. Hukumu yake iliungwa mkono na mahakama ya rufaa na mahakama kuu licha ya kwamba hakukuwa na ushahidi wowote wa kumuharibia jina waziri mkuu. Mahakama imemtoza faini bi Sochua na kumpa fidia waziri mkuu, amepewa hadi Julai 16 kulipa faini hiyo ambayo Bi Sochua amekataa kulipa.