Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watumishi sita wa UM wauawa na bomu la kujitolea mhanga Kabul

Watumishi sita wa UM wauawa na bomu la kujitolea mhanga Kabul

Taarifa za Idara ya Habari ya UM zimeeleza kwamba watumishi 6 wa UM walikuwa miongoni mwa watu 12 waliouawa kwenye shambulio la bomu la kujitoa mhanga, liliofanyika mapema Ijumatano, katikati ya mji wa Kabul, Afghanistan, kwenye nyumba ya wageni inayotumiwa na wafanyakazi wa UM.

Ripoti zilisema watu kadha walijeruhiwa. Kai Eide, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Afghanistan na Mkuu wa Shirika la UM la Kuongoza Misaada katika Afghanistan (UNAMA), aliwaambia waandishi habari waliopo Kabul kwamba shambulio la mastakimu ya wafanyakazi wa UM "halitopunguza, hata kidogo, hamasa ya watumishi wa kimataifa kutekeleza majukumu waliodhaminiwa nayo, kuisaidia Afghanistan kufufua shughuli za uchumi na huduma za jamii, kwa minajili ya kustawisha taifa lilioghumiwa na mapigano ya muda mrefu;" na aliongeza kusema UM utahakikisha "WaAfghani wote watapatiwa fursa ya kustarehea maisha bora, yenye utulivu na amani, kwa siku zijazo." KM Ban Ki-moon akijumuika na Mjumbe Maalumu wake kwa Afghanistan, Kai Eide walishtumu vikali, kwa pamoja, hii leo, shambulio la wafanyakazi wa UM. Katibu Mkuu, kwa upande wake, alisema shambulio dhidi ya wafanyakazi wa UM, waliopoteza maisha leo mjini Kabul, kilikuwa ni kitendo cha "kushtusha na kisio aibu;" alisema watumishi wa UM waliporidhia kwenda Afghanistan, kulisadia taifa kurudisha utulivu na amani, walikwenda huko bila ya kuchukua silaha za bunduki, wala risasi. Lakini walichukua silaha nyengine, "yenye nguvu zaidi" alisema KM, akimaanisha silaha ya kuupa umma wa Afghanistan "matumaini na tegemeo" ya kwamba "maendeleo bora yapo njiani kuwasili nchini mwao, na waliahidi kuusaidia umma kujenga maisha mema kwa siku za baadaye."