Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Alain Le Roy, Naibu KM wa Idara ya Operesheni za Ulinzi Amani za UM (DPKO) amezuru Abuja, Nigeria Alkhamisi ikiwa miongoni mwa maeneo anayozuru katika Afrika Magharibi. Alifanya mazungumzo na maofisa wanaohusika na masuala ya nchi za kigeni, maofisa wanaowakilisha wizara ya ulinzi pamoja na kukutana na Mshauri Mkuu wa Masuala ya Usalama wa Taifa. Vile vile alionana na Rasisi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Uchumi wa Mataifa ya Afrika Magharibi, Dktr Mohamed Ibn Chambas.

Hii leo kulitangazwa taarifa ya pamoja, kutoka Nairobi, ya kulaani kwa kauli kali, shambulio la bomu la kujitolea mhanga liliogeshwa ndani ya gari, liliofanyika kwenye mji wa Beledwenye, Usomali ambapo Waziri wa Usalama, Omar Hashi Aden aliuawa pamoja na viongozi wa jamii na Wasomali wengine wasio hatia. Taarifa iliwakilishwa kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Shirika la Uhusiano Miongoni-mwa-Serikali juu ya Maendeleo, Umoja wa Mataifa Huru ya Kiarabu na pia Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali na kusema shambulio hilo lilikuwa ni la kuchikiza na limebainisha tena, wazi kabisa kwamba wafuasi wa vile vikundi vyenye siasa kali waliopo Usomali, na wasio na matumaini, wanaojumlisha wazalendo na wageni, wapo tayari kufanya kila wawezalo, kujaribu kunyakua madaraka kwa mabavu, kutoka serikali halali ya Usomali. Taarifa iliisihi serikali isiingiwe na wasiwasi kutkana na uhalifu wa kutumia mabavu ulioendelezwa na walio wachache dhidi ya madaraka yao. Serikali ilihimizwa iendelee na jitihadi zake za upatanishi na kurudisha amani nchini, kama ilivyopendekezwa na Maafikiano ya Djibouti.

Asubuhi KM Ban Ki-moon alihutubia mkutano wa Baraza Kuu uliosailia "ufanisi wa matumizi ya nishati, hifadhi bora ya nishati na vyanzo vipya vya nishati na vile vya kutumiwa mara kwa mara." Kwenye maelelzo yake, KM alisihi kwamba mafanikio makubwa yataweza kupatikana pindi umma wa kimataifa utahimizwa kutumia nishati, kwa ufanisi, hatua ambayo ikitekelezwa anaamini itapunguza tatizo la kumwaga hewa chafu kwenye anga, gharama za kutumia nishati kwenye shughuli za biashara na katika majumba, na itatupatia fursa ya kuzalisha ajira ziada. Alisema kuna haja kwa serikali za kimataifa kwa sasa kubuni sera mpya, zenye nguvu, zenye lengo la kudhibiti bora nishati, hasa ilivyokuwa sekta zote za jamii zinahitajia matumizi ya ufanisi wa nishati, hali ambayo itakuza huduma safi za maendeleo na kuyasaidia mataifa kukabili, kwa mwelekeo mmoja, yale matatizo yanayoletwa na mabadiliko ya hali ya hewa na bei za kigeugeu za nishati na, hatimaye, kupunguza umaskini na ufukara.

Staffan de Mistura, mkuu wa Shirika la UM la Usaidizi Amani Iraq (UNAMI), ambaye anakaribia kumaliza muda wa kazi, leo asubuhi alihutubia Baraza la Usalama, kwa mara ya mwisho, kama kiongozi wa UNAMI. Alipongeza mchango muhimu wa UM wa kuisaidia Iraq "kuwa taifa lenye utawala huru na wenye utulivu." Alitoa mfano wa mchango wa UM katika kupatanisha makundi kadha yaliohasimiana, kwa kuruhusu mlango wa majadiliano kuwa wazi ili kuendeleza mawasiliano ya amani, hususan baina ya Waarabu na Wakurdi wa Iraq. Aliongeza kusema ya kuwa Iraq mwaka huu imefanikiwa kufika kwenye njia panda kihistoria kuhusu matukio ya uchaguzi, na ni matumaini yake uchaguzi wa taifa katika kipindi kijacho utaendelezwa kwa utulivu unaostahiki. Wakati huo huo UM unaendelea kulisaidia taifa kujenga uwezo madhubuti wa kudhibiti vyema madaraka. De Mistura aliwaambia wajumbe wa Baraza la Usalama "awamu ijayo ya utawala inabashiria Iraq itashuhudia maendeleo yenye matumaini, yatakayoendelea kupanuka kwa wastani."

Ripoti mpya ya KM kuhusu hali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (JAK), iliowakilishwa Alkhamisi, imetahadharisha nchi sasa imefikia kipindi cha kufanya maamuzi muhimu juu ya maendeleo, na inahitajia kuhudumiwa misaada ya dharura na jumuiya ya kimataifa kuiwezesha kupunguza umaskini wa mwisho uliotanda kitaifa kwa sasa. Kuhusu matayarisho ya uchaguzi mkuu ujao wa 2010, ripoti ilisisitiza ratiba ya tukio hilo ni lazima ihishimiwe na wahusika wote nchini. Kadhalika, kwenye ripoti KM alisema ameingiwa na wasiwasi juu ya watu kuendelea kufanya makosa ya jinai nchini bila ya kukhofu adhabu, na pia alisema ana wahka kuhusu hali ya usalama, unaoregarega, kwenye lile eneo la mpakani baina ya JAK, Chad na Sudan linalojulikana kwa umaarufu kama "eneo la pembetatu la vifo", sehemu ambayo JAK haina uwezo wa kudhibiti matatizo ya usalama na yale yanayohusu kukatiza mipaka kusio halali. Alitumai ofisi ya taasisi za pamoja za UM kuimarisha amani itakapofunguliwa katika JAK itasaidia kuwakilisha maendeleo yanayotakikana, hasa baada ya Baraza la Usalama kupitisha mapendekezo yote ya KM kuhusu JAK.

Shirika la UM juu ya Amani Sudan Kusini (UNMIS) limeripoti wanajeshi 5,000 wanaojumuisha askari wa Jeshi la Sudan, pamoja na wale wa kundi la waasi la SPLA na kutoka majeshi ya mgambo ya kundi la PLA, liliokuwa likiunga mkono Serikali, wamefanikiwa kupokonywa silaha na kuunganishwa na maisha ya jamii za kikawaida. Maafikiano ya Amani ya Jumla (CPA) yalisisitiza kwamba suala la kupokonywa silaha wale wapiganaji wa zamani ndio tukio muhimu la kimsingi liliowezesha mapigano kusimamishwa baina ya makundi yaliohasimiana ya kutoka kaskazini na kusini. UNMIS imearifu mradi wa kuwapokonya silaha wanajeshi wanaokadiriwa 180,000 pamoja na wanawake walioshirikiana nao kwenye mapigano, ulikuwa ni mpango mgumu kuutekeleza kwa matumaini ya kuurejesha umma huo katika maisha ya raia wa kawaida. Kadhalika wapiganaji watoto nao pia walitazamiwa kurudishwa kwa aila zao kulingana na maafikiano ya CPA.

Mahakama Maalumu juu ya Makosa ya Vita katika Sierra Leone imetangaza kesi ya aliyekuwa raisi wa Liberia Charles Taylor inatazamiwa kuanza rasmi tarehe 13 Julai, na wakili wa utetezi wameombwa wajiandae kuwasilisha hoja zao na ushahidi walionao mnamo tarehe hiyo, ambaye ilibadilishwa kutoka tarehe ya zamani ya 13 Juni. Mashitaka ya awali yatasikilizwa Julai 06 kwenye jengo la Mahakama ya Kimataifa juu ya Jinai ya Halaiki (ICC) iliopo kwenye mji wa Hague, Uholanzi.

Baraza la Haki za Binadamu Alkhamisi limemaliza kikao cha kawaida, cha 11 mjini Geneva ambapo maazimio 15 yalipitishwa, ikijumlisha yale masuala yanayohusu haki za kimsingi za wahamaji waliopo kwenye vituo vya kufungia watu vya idara ya wahamiaji; pendekezo la kuharakisha juhudi za kukomesha, halan, hali yote ya kutumia mabavu dhidi ya wanawake, na kukomesha utoroshaji wa watu wanaolazimishwa kushiriki kwenye ajira haramu nje ya makwao, na kuzingatia Mswada wa Kanuni za Uongozi juu ya kuondosha umaskini mkubwa, na maazimio yanayohusu utekelezaji wa haki za binadamu. Baraza hilo vile vile limeamua kuandaa mfumo wa madaraka maalumu ya mwaka mmoja atakayokabidhiwa nayo mtaalamu huru atakayeshughulikia masuala ya haki za binadamu katika Sudan.