Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti ya kuwa itamudu kukidhi mahitaji ya msingi ya chakula kwa wahamiaji wa ndani (IDPs) milioni 2.6, katika miezi ya Juni na Julai, waliopo kwenye maeneo ya mapigano katika Pakistan. UM inasema umepokea asilimia 43 tu ya zile fedha zinazotakikana kuhudumia mahitaji hayo, kati ya jumla ya dola milioni 280 ya maombi ya chakula. Kadhalika, akiba ya madawa muhimu inatazamiwa kumalizika katika mwisho wa mwezi, na misaada ya dharura itahitajika kuhudumia afya ya umma mnamo miezi sita ijayo. Halkadhalika, imeripotiwa kuwepo upungufu mkubwa wa vifaa vya huduma ya afya pamoja na ukosefu wa sabuni kwa watu waliopo kwenye kambi za IDPs. Vile vile Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti kwamba kati ya mama wajawazito 50,000, wanaotarajiwa kuzaa katika miezi sita ijayo, wajawazito 5,000 wanakadiriwa watahitajia kupelekwa hospitali kupata matunzo ya dharura mazuri juu ya uzazi.

Maofisa wa zamani wa kijeshi, wa vyeo vya juu, kutoka Usomali, kuanzia Ijumatano watakutana kwa muda wa siku mbili kwenye mji wa Washington D.C. kushauriana kipamoja kuhusu ulinzi na usalama wa taifa lao, ambapo mapigano yaliselelea huko kwa muda mrefu. Mkutano umeandaliwa na Ofisi ya UM juu ya Masuala ya Kisiasa katika Usomali na utaongozwa na Wizara ya Ulinzi ya Usomali. Kwa mujibu wa Mjumbe Maalumu wa KM kwa Usomali, Ahmedou Ould Abdallah wanajeshi wa zamani wa Usomali "wanahishimiwa sana kutokana na uzoefu wa kitaalamu walioupata katika kipindi cha historia ya Usomali, ujuzi ambao ulitumiwa hata na mataifa mengine ya Afrika katika kuwafunza wanajeshi wao."

Kadhalika, Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) limeanzisha mafunzo maalumu mjini Kinshasa kwa polisi 2,500 wa Kongo, wanaotazamiwa kusaidia kuimarisha usalama wa umma wakati wa uchaguzi ujao wa mitaa nchini humo. Ratiba ya mafunzo inajumlisha mafundisho juu ya namna ya kukusanya ushahidi, kudhibiti utulivu wa wapiga kura kwenye vituo vya kupiga kura, na katika kusafirisha na kulinda vifaa vya kura. Baada ya mafunzo haya polisi wa JKK wataenezwa kwenye vituo 143 vya usajili wa kura kwenye mji wa Kinshasa. Wiki ijayo maofisa wa polisi kutoka jimbo la Bas-Kongo nao pia watapatiwa mafunzo juu ya ulinzi wa umma wakati wa uchaguzi wa mitaa. Kadhalika, katika wiki zijazo UM utawapatia mafunzo haya muhimu maofisa wazalendo 75,000 wa JKK. Kwa mujibu wa MONUC, kuanzia mwisho wa wiki orodha mpya ya wapigakura itatangazwa rasmi nchini.

Juan Somavia, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa juu ya Haki za Wafanyakazi (ILO) kwenye risala yake hii leo mbele ya kikao cha mwaka cha bodi la utawala mjini Geneva, alitoa mwito wa kuwepo mfumo wa uchumi wa kimataifa unaosarifika na ulio wa haki ambapo natija zake zitazalisha shughuli za kudumu na Ajira Stahifu. Somavia alishtumu sera za mfumo wa uchumi uliotawala sasa hivi kimataifa ambao, alisisitiza, ndio uliozusha migogoro ya kifedha kwenye soko la kimataifa, kwenye mazingira ambayo yaliamua kupuuza kabisa maadili ya kustawisha na kuimarisha haki za wafanyakazi. Anakhofia juhudi za kuhifadhi ajira na jamii zitazorota katika miaka sita hadi minane ijayo, na alitahadharisha ya kuwa ukosefu wa ajira na ruzuku kwa jamii isiojiweza huenda ikazalisha vurugu na fujo katika maeneo kadha wa kadha ya ulimwengu.