Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisa wa ECA ameripoti taaluma ya sayansi Afrika ndio ngao dhidi ya migogoro

Ofisa wa ECA ameripoti taaluma ya sayansi Afrika ndio ngao dhidi ya migogoro

Wataalamu wa sayansi 600 kutoka sehemu mbalimbali za dunia wamekusanyika wiki hii Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria Kikao cha Awali cha Kamati ya Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia (CODIST-1) kilichoanza mashauriano leo Alkhamisi.

 Josué Dioné, Mkurugenzi wa Kitengo cha Baraza la Uchumi Maendeleo kwa Afrika (ECA), anayehusika na Masuala ya Kuimarisha Chakula na Maendeleo ya Kusarifika, alinasihi kwenye risala ya ufunguzi kwamba serikali za Afrika zinawajibika kuchangisha msaada maridhawa wa kizalendo, utakaotumiwa kwenye utafiti wa kuvumbua teknolojia mpya inayohitajika kuchochea maendeleo ya kudumu kwenye eneo lao, kadhia ambayo anaamini ikitekelezwa kama inavyostahiki itazikinga nchi za Afrika na madhara yanayotokana athari za mizozo ya uchumi, inayojiri mara kwa mwara kwenye soko la kimataifa. Alitoa mfano wa mataifa ya Uchina na Bara Hindi kuyakinisha hoja yake, nchi ambazo alisema zimemudu miradi ya kukuza ilimu ya sayansi na teknolojia ya kizalendo, kwa kiwango kilichosaidia kukuza haraka maendeleo yenye natija kwa fungu kubwa la umma wao.