Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Jumuiya ya Mashirika ya UM Dhidi ya UKIMWI (UNAIDS) imekaribisha uamuzi wa Bunge la Burundi la kukataa ule mswada wa sheria ya kuharamisha usenge na ukhanithi nchini. Michel Sidibé, Mkurugenzi Mkuu wa UNAIDS amewasifu Wabunge kukataa marekibisho hayo, na anaamini kuwa wameonyesha ari kuu ya kutunza haki za binadamu za umma wao, kitendo ambacho anahisi ni cha kupigiwa mfano kwa wabunge wengine wa kimataifa. Kwa mujibu wa taarifa ya UNAIDS, uharamishaji wa tabia ya kijinsiya ya wanaume watu wazima na utenguzi wa haki za binadamu za watu wenye kuishi na virusi vya UKIMWI, ni mambo yenye kukwamisha juhudi za kudhibiti bora maambukizi ya VVU katika dunia, ambazo zinafungamana na fedheha ya uhalifu dhidi ya wasenge.

Susanna Malcorra, Naibu KM juu ya Misaada ya Wahudumia Amani sasa hivi yupo Khartoum akihudhuria mkutano wa pande tatu, ulioshirkisha UM, Serikali ya Sudan na pia wawakilishi wa Umoja wa Afrika, ikiwa katika juhudi za kuhakikisha vikosi vya mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) vitaendelea kupelekwa kwenye eneo husika bila ya matatizo kuongoza shughuli zao, pamoja na vifaa vyao. Kikao hiki kitakuwa ni cha nne na kitazingatia namna ya kurahisisha huduma hizo bila vizingiti. Kadhalika, maofisa wa vyeo vya juu wa UM wameahidiwa na Naibu Gavana wa Darfur Kusini kuwa wataendelea kuruhusiwa kwenda kwenye eneo la Muhajariya na sehemu za jirani na hapo bila yamatatizo. Mkuu wa misaada ya kiutu katika Sudan, Ameerah Haq alishiriki pia kwenye mazungumzo maalumu na wenye madaraka yaliosaidia kuhakikisha watu 100,000 muhitaji watahudumiwa, kwa wakati, ile misaaada ya kihali inayotakikana kunusuru maisha.

Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) limetangaza ripoti ilioshtumu vikali vitendo vya waasi wenye asili ya Kihutu, wa kundi la FDLR ambavyo vilikiuka sheria dhidi ya raia wa eneo la mashariki katika JKK. MONUC inasema waasi hawa wa FDLR hutumia vitisho vya mpangilio na ukatili dhidi ya raia, mathalan, huiba mali za raia, na mara nyengine huwateka nyara na kuwanajisi kimabavu, na baadaye huwaua raia mateka. MONUC imelaani vitendo hivi ambavyo ilisema ni "mbinu za kigaidi na za waoga", nha humaanisha waasi wa FDLR wamenuia kudhoofisha operesheni za pamoja za vikosi vya Rwanda na JKK vya kuwatoa mafichoni na kuwafukuza nchini. Mashambulio ya FDLR dhidi ya raia pia yamekusudiwa kuzorotisha uwezo wa Serikali kudhibiti bora utawala kwenye eneo la uhasama la kaskazini-mashariki katika JKK.  Kwa sababu hizo MONUC ilianzisha timu maalumu za kuhakikisha raia wanapatiwa hifadhi, timu ambazo zimeenezwa kwenye kambi za majeshi ya kulinda amani, ambapo walinzi wa UM pia hufanyisha doria ya saa ishirini na nne inayohakikisha umma husika unapatiwa hifadhi wanayostahiki kisheria.