Hapa na Pale

Hapa na Pale

Kwenye taarifa iliotolewa Ijumaa kwa waandishi habari, na Shirika la UM juu ya Ulinzi wa Amani katika JKK (MONUC) ilimnakili Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM kwa JKK akisema “Tumearifiwa Jenerali [Laurent] Nkunda ameshikwa” , na kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Uongozi wa Operesheni za Pamoja kitendo cha kumkamata Nkunda kilifanyika “ndani ya Rwanda.” Doss alisema Baraza la Usalama la UM liliwanasihi, mara chungu nzima, Nkunda na kundi lake la waasi la CNDP, kufuata utaratibu wa majadiliano kusuluhisha mzozo waona Serikali ya JKK. Alitumai wafuasi wa CNDP hivisasa watatumia fursa walionayo kujiunga na jeshi la taifa na, hatimaye, kuhakisha amani kurudishwa na kudumishwa katika eneo la Kivu.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Kiutu ya Dharura (OCHA) ikijumuika na Ofisi ya Mratibu Maalumu wa UM juu ya Mpango wa Amani katika Mashariki ya Kati (UNSCO) zimeripoti kuwasili kwenye Tarafa ya Ghaza Ijumaa, timu ya wataalamu wa kuondosha mabomu yaliotegwa ambayo bado hayajaripuka. Timu itatathminia utaratibu wa kuharakisha ufyekaji wa silaha hizo ili kurahisisha ugawaji wa misaada ya kiutu katika Ghaza. Wakati huo huo, skuli zote zinazosimamiwa na Shirika la UNRWA katika Ghaza zinatarajiwa kufunguliwa Ijumamosi (24/01/2009). Moja ya shughuli muhimu zitakazoongozwa na skuli za Ghaza, mnamo wiki ya kwanza baada ya kufunguliwa, ni kuhakikisha mahitaji ya kiakili na kijamii ya wanafunzi watoto yanatekelezwa, kabla ya kuanzisha masomo. Skuli za Ghaza zilitarajiwa kufunguliwa tarehe 17 Januari lakini zilichelewa kufunguliwa kwa sababu ya vita.

Ofisi ya Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, ikijumuika na Shirika Linalosimamia Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) imetangaza ripoti ya pamoja kuhusu mauaji ya raia 33 na majeruhi 108 waliokuwa katika kambi ya wahamiaji wa ndani ya Kalma, Sudan Kusini, msiba uliotukia tarehe 25 Agosti 2008. Ripoti ilisema imethibitisha, kufuatia uchunguzi wao, ya kuwa vikosi vya usalama vya Serikali ya Sudan vilikiuka sheria ya kiutu ya kimataifa kwa kutumia mabavu ya kuua, kwenye mazingira “yasiostahiki utumiaji wa silaha au nguvu zisiowiana na makosa yanayodaiwa yalifanyika kambini.” Ripoti ilisema kitendo cha vikosi vya usalama vya Sudan katika kambi ya Kalmi vilikuwa ni “haramu.”

Ripoti mpya juu ya mripuko wa maradhi ya kipindupindu katika Zimbabwe, iliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) Ijumaa inasema hali bado haijadhibitiwa kidharura kama inavyotakikana, na maambukizo yanaendelea kukithiri katika nchi. Idadi ya wagonjwa wa kipindupindu waliosajiliwa kwa sasa ni 50,000 ziada, na kati ya jumla hiyo watu 2,773 walishafariki kutokana na janga hilo. Kwa mujibu wa WHO wiki ya baina tarehe 17 mpaka 17 Januari 2009 kulisajiliwa idadi kubwa ya vifo pamoja na watu walioambukizwa kipindupindu katika Zimbabwe.

Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kuwa mwaka jana lilinunua idadi kubwa ya chakula kutoka mataifa ya kusini mwa Afrika. WFP iliripoti tani za metriki 550,000 za chakula zilinunuliwa kutoka mataifa ya Afrika Kusini, Msumbiji, Malawi na Zambia. Chakula hiki kinatarajiwa kugaiwa watu, karibu milioni tatu, kwa mwaka mmoja mfululizo katika mataifa muhitaji ya kusini mwa Afrika na pia kwenye maeneo mengine ya Afrika panapozuka dharura.