Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNRWA inasema inaongeza bidii kuhudumia kihali waathirika wa mashambulio katika Ghaza

UNRWA inasema inaongeza bidii kuhudumia kihali waathirika wa mashambulio katika Ghaza

John Ging, Mkurugenzi wa Opereshini za Shirika la UM Linalofarajia Misaada ya Kihali kwa WaFalastina wa Mashariki ya Karibu (UNRWA) alizungumza na waandishi habari Ijumaa asubuhi mjini Geneva, kwa kupitia njia ya simu kutokea Ghaza, ambapo alibainisha ya kuwa Israel bado haijaruhusu kufunguliwa vile vivuko ambavyo hutumiwa na malori yanayochukua bidhaa, na misaada ya kihali, ya kuhudumia umma wa Tarafa ya Ghaza.

“Hivi sasa, hapa Ghaza tumelenga huduma zetu, kusaidia waathirika wa mashambulio ya karibuni kumudu huzuni walizonazo, na pia kukabili uharibifu mkubwa uliolifunika eneo lao .. masuala mawili muhimu sana ambayo ni lazima kushughulikiwa kidharura na jumuiya ya kimataifa ili kuwaponya wakazi wa Ghaza na maafa waliopitia.” Alisema wale ambao jamaa zao waliuawa, au kujeruhiwa na mashambulio ya mabomu na makombora ya vikosi vya uvamizi vya Israel, wamo kwenye huzuni kubwa. Alieleza kwamba msiba waliopitia wakazi wa Ghaza ni wa kuduwaza akili, bila ya shaka, na madaktari wamethibitisha kihakika kwamba sasa hivi wingi wa wakazi wa Ghaza wanateseka na maradhi ya akili yanayochochewa na mishtuko wakati wa vita na vurugu. Alienedelea kusema mkuu huyo wa UNRWA ya kuwa asilimia kubwa ya waathirika wamekasirika na kughadhibika hadi, na vile vile wamepoteza imani kwamba watapatiwa haki pindi wakisubiri na kutegemea utaratibu wa sheria za kimataifa. Ging alisema UNRWA inajitahidi kuwapoza na kuwafahamisha WaGhaza kwamba UM utaendelea kusisitiza ya kuwa wale wote waliohusika na uharibifu na makosa yaliokiuka sheria ya kimataifa, dhidi ya wakazi wa Tarafa ya Ghaza, kutoka vikosi vya Israel, watafikishwa mahkamani kukabili haki baada ya kuthibitishwa makosa yao.