Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Vikosi Mseto vya UM/UA vya Kulinda Amani Darfur (UNAMID) vimearifu askari 45 wa Kombania ya Usafiri Wastani ya Jeshi la Ethiopia waliwasili karibuni katika Darfur Magharibi. Kombania hii ya majeshi ya Ethiopia itatumiwa kugawa shehena za mizigo na vifaa baina ya kambi za walinzi wa amani wa UNAMID, ikijumlisha ugawaji wa maji na matangi ya nishati, na vile vile kuwapatia wanajeshi usafiri.

KM Ban Ki-moon alituma salamu za taazia, kwa aila na kwa umma, kwa ujumla baada ya kuarifiwa kifo cha Jenerali Lansana Conté, Raisi wa Jamhuri ya Guinea kilichotukia Ijumatatu. Kwenye risala yake KM alisema Raisi Conté alikuwa kiongozi aliejihusisha, kwa muda mrefu sana, katika kutekeleza ahadi za kuimarisha umoja na amani nchini mwao, na pia kuendeleza utulivu na ushirikiano wa kikanda kwenye eneo la Bonde la Mto Mano. Vile vile KM alipongeza ukarimu wa taifa la Guinea, chini ya uongozi wa marehemu Raisi, kwa kuwapokea mamia elfu ya wahamiaji waliohajiri makwao kunusuru maisha na kukwepa mapigano yaliojiri kwenye nchi jirani. Kadhalika, KM alisisitiza kwenye risala yake kwamba katika kipindi cha mabadiliko kuna haja kuu ya kuhakikisha madaraka yanahamishwa kwa njia ya amani, yenye kufuata mfumo wa kidemokrasia, kwa kulingana na Katiba halali ya nchi. Ametoa mwito wa kuhimiza hali tulivu nchini, na alisihi vikosi vya taifa pamoja na wadau wengineo husika, kuhishimu utaratibu wa kidemokrasia nchini katika wakati wa mageuzi.

Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) imeripoti kuwa na ushahidi, wenye kuaminika kidhati, kuhusu muongezeko wa wapiganaji waasi wa kundi la CNDP, linaloongozwa na Laurent Nkunda, katika barabara maalumu, hali ambayo imevilazimisha vikosi vya MONUC katika eneo la Masisi kujitayarisha kwa mapambano, na kuongeza doria ziada katika zile sehemu muhimu za eneo lao. MONUC vile vile imeripoti kuwa na wahka kutokana taarifaza mapambano kuzuka Ijumanne baina ya waasi wa CNDP na na vikosi vya kikabila vya jeshi la mgambo la Mai Mai. Makundi yote yenye silaha yamenasihiwa kujizuia na vitendo vya kupanua vikosi vyao ili wasije wakachochea khofu na kusababisha raia kuhajairi tena makwao. MONUC pia imesihi makundi yote kujizuia na vitisho vya kutumia mabavu na nguvu dhidi ya wale wanaohasimiana nawo.