Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisa mkaazi wa WHO anasema "hali ni ngumu tangu mashambulio kuanzishwa Ghaza"

Ofisa mkaazi wa WHO anasema "hali ni ngumu tangu mashambulio kuanzishwa Ghaza"

Leo asubuhi tulipata taarifa ziada kutoka Mahmoud Daher, Ofisa wa Afya anayewakilisha Shirika la Afya Duniani (WHO) katika Ghaza, ambaye alihojiana, kwa kutumia njia ya simu, na Samir Imtair Aldarabi, mwanahabari wa Idhaa ya Kiarabu ya Redio ya UM. Daher alielezea hali ilivyo sasa hivi katika Ghaza, kama ifuatavyo:~

“Hali katika Ghaza ilianza kuharibika zaidi kufuatia operesheni za kijeshi za vikosi vya Israel zilizoanzishwa Ijumamosi adhuhuri .. na tangu wakati huo hadi hii leo, WaFalastina 310 wameshauawa .. na idadi hiyo inajumlisha watoto 15 na wanawake kadha, na watu 1200 walijeruhiwa, wingi wao wakionekana kuelekea kwenye wodi za mejeruhi .. 74 ya idadi hiyo wapo katika hali mbaya kabisa, na 43 yao wamo kwenye kitengo cha wagonjwa maututi, na asilimia 21 ya majeruhi waliosajiliwa na WHO walikuwa ni watoto wadogo, na pia kulisajiliwa majeruhi wanawake 168.” Ofisa wa WHO alisema, kikawaida, huduma za afya katika Hospitali ya Wizara ya Afya zimeshatumiwa bila ya kiasi, na sasa hivi kuna upungufu mkubwa wa aina 105 ya madawa, na pia upungufu wa vifaa muhimu 225 vinavyohitajika kutumiwa na wagonjwa na wahudumia afya. Hali hii, alisisitiza, ndio yenye kuchangisha matatizo magumu kwenye huduma za afya mahospitalini na kuzorotisha huduma za dharura za afya, kwa umma muhitaji.